1 Kings 22:1-28

Mikaya Anatabiri Dhidi Ya Ahabu

(2 Nyakati 18:2-27)

1Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli. 2Lakini katika mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme wa Yuda akashuka kwenda kumwona mfalme wa Israeli. 3 aMfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?”

4 bKwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?”

Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”
5 cLakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta shauri la Bwana.”

6 dKwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?”

Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”

7 eLakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Bwana hapa ambaye tunaweza kumuuliza?”

8 fMfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia yeye twaweza kumuuliza shauri la Bwana, lakini namchukia kwa sababu huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu mimi, lakini kila mara hunitabiria mabaya tu. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.”

Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”

9Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”

10Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao. 11 gWakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma, akatangaza, “Hivi ndivyo Bwana asemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’ ”

12Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa Bwana ataitia mkononi mwa mfalme.”

13Mjumbe aliyekuwa amekwenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”

14 hLakini Mikaya akasema, “Hakika kama Bwana aishivyo, nitamwambia kile tu Bwana atakachoniambia.”

15Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?”

Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa Bwana atawatia mkononi mwa mfalme.”

16Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la Bwana?”

17 iNdipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema, ‘Watu hawa hawana bwana. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ”

18Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, bali mabaya tu?”

19 jMikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la Bwana: Nilimwona Bwana ameketi juu ya kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama kumzunguka upande wa kulia na wa kushoto. 20Naye Bwana akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’

“Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile.
21Mwishoni, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele za Bwana na kusema, ‘Nitamshawishi.’

22 kBwana akauliza, ‘Kwa njia gani?’

“Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’

Bwana akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’

23 l“Kwa hiyo sasa Bwana ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Bwana ameamuru maafa kwa ajili yako.”

24Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Bwana alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”

25 mMikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapokwenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”

26Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni na mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme. 27 nMkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji mpaka nitakaporudi salama.’ ”

28 oMikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Bwana hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”

Copyright information for SwhNEN